Leo, 26 Machi 2025, wajumbe kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wakiwemo Mhandisi Hanington Kagiraki, Msanifu Majengo Dickson Haule na Mkadiriaji Majengo Geofrey Nyaluke, wametembelea na kufanya ukaguzi wa ujenzi wa mabweni unaoendelea katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mwanza.
Mabweni hayo, yanayojengwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET), yatahudumia wanafunzi wa kike 200 na wa kiume 100, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha wanafunzi wanapata makazi bora na salama.
Wakiwa katika eneo la ujenzi, wajumbe hao walifanya kikao na mkandarasi wa mradi, China National Aero Technology International Engineering Corporation, ili kufuatilia maendeleo na kuhakikisha kuwa ujenzi unakidhi vigezo na viwango vilivyowekwa.
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kusisitiza umuhimu wa ubora katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo mabweni haya ambayo yataboresha ustawi wa wanafunzi wa Kampasi ya Mwanza.
Ukaguzi huo umelenga kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa kwa ufanisi, kwa kuzingatia muda uliopangwa na viwango vinavyotakiwa, ili kufanikisha dhamira ya serikali ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.