Leo, tarehe 16 Januari 2025, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA na Mwenyekiti wa Baraza Dogo la Wafanyakazi, Profesa William Pallangyo, amefungua kikao cha tano cha Baraza Dogo la Wafanyakazi wa Kampasi ya Dar es Salaam kilichofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Profesa Pallangyo amewakumbusha wafanyakazi kuwa lengo la Baraza ni kuwakutanisha wafanyakazi na waajiri kwa ajili ya kujadili masuala muhimu ya kazi na mazingira yao,
“Ubunifu ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu yetu. Niwasihi kuendelea kujifunza ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia,”. Alisisitiza Profesa Pallangyo
Pia, ametoa wito kwa Kurugenzi ya Utawala kuhakikisha kuwa mafunzo yanatolewa mara kwa mara kwa watumish na kuboresha mshikamano miongoni mwa wafanyakazi ili kuimarisha utendaji kazi wa taasisi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam), Dkt. Momole Kasambala, alieleza mafanikio ya mashindano ya ubunifu wa mawazo ya kibiashara yaliyoandaliwa kwa wanafunzi wa kampasi zote za TIA,
“ Mashindano hayo yalizinduliwa tarehe 31 Oktoba 2024 katika Kampasi ya Mbeya na kufikia kilele chake tarehe 12 Desemba 2024 katika Kampasi ya Dar es Salaam,”. Alisisitiza Dkt.Kasambala
Washindi wa mashindano hayo walipewa zawadi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ziara ya mafunzo nchini Uganda katika Chuo Kikuu cha Makerere, inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Januari 2025, ambapo ziara hiyo inalenga kuwajengea wanafunzi maarifa zaidi kuhusu mbinu za ubunifu na ujasiriamali.