Ugeni huo uliongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo, ambaye alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi hizo katika kusaidia wanafunzi wa TIA pamoja na jamii kwa ujumla. Prof. Pallangyo alibainisha kuwa ushirikiano huo utaendelea kuchochea mafanikio kupitia kauli mbiu ya mbio hizo: “Run, Inspire and Support.”
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa YAS, Bw. Norman Kiondo, aliupokea ugeni wa TIA na kushiriki mazungumzo yenye lengo la kuimarisha mahusiano na kuboresha maandalizi ya TIA Marathon 2025. Mazungumzo hayo yalijikita katika kubainisha mbinu bora za kuendeleza ushirikiano baina ya taasisi hizo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
TIA Marathon 2025, msimu wa pili, imepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa na dhamira ya kuhamasisha, kuunga mkono na kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Kupitia tukio hili, TIA na YAS zinalenga kuendelea kuchangia katika ustawi wa jamii na kutoa huduma bora zaidi kwa taifa na wadau wao.

