TAMASHA LA MICHEZO LA WANAFUNZI WA TAASISI YA UHASIBU SINGIDA LAFUNGULIWA

May 18, 2022
Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida imeanza rasmi wiki ya michezo huku ikitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Umma wa watanzania na vijana waliohitimu kidato cha nne mwaka 2021 na miaka ya nyuma kujiunga na TIA kwa ajili ya masomo kwa ngazi ya cheti yaani “Certificate” na Diploma kwa mwaka 2022/2023 baada ya Taasisi hiyo kufungua dirisha la maombi.
Akizungumza  kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Profesa. William Amos Pallangyo Meneja wa TIA Kampasi ya Singida Dkt.James Mrema alielezea  namna ya kujiunga na masomo katika Chuo cha TIA kwa Mwanafunzi mwenye ufaulu kuanzia alama D4 anaweza kutuma maombi yake kwani atakuwa amekidhi sifa za kujiunga na dirisha liko wazi tangu Mei 14 hadi 15 Agosti 2022
“Nawakaribisha kujiunga na programu za fani ya Uhasibu na Fedha, Uhasibu wa Umma, Ugavi na manunuzi, Usimamizi Rasilimali Watu, Masoko na Uhusiano wa Umma, Usimamizi wa Biashara. Fomu za maombi zinapatikana katika tovuti ya taasisi www.tia.ac.tz au unaweza kufika chuoni na kujaza fomu, pia unaweza kupata fomu hizo katika shule za sekondari walikohitimu kidato cha nne,”. Alisisitiza Dkt.Mrema
Awali akifungua michezo hiyo jana kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Kizigo  aliwataka wanafunzi wa chuo hicho kutumia michezo hiyo kupata fursa mbalimbali za kuwainua kiuchumi na sio kuwa “memory card’
“Tumieni michezo kama sehemu ya kuwaleta pamoja kutambua na kupata fursa mbalimbli zilizopo kwenye jamii ili muinuke kiuchumi na si kuwasindikiza wenzenu kwani kupitia michezo itawasaidia kuzitambua fursa mbalimbli zikiwemo za kiuchumi,”. alisema DC Kizigo.
Mkuu wa Wilaya Mhe.Sophia Kizigo aliwakumbusha Wana Singida kuhakikisha wanajitokeza kuhesabiwa kwani ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Tamasha hili  limelenga kuwajengea wanafunzi mazoea ya kupenda michezo ili kutanua ubongo, kulinda afya ya kiakili na kutia chachu katika kupambana na mawazo hasi na kuruhusu kuwaza katika mlengo chanya ambapo michezo mbalimbali kama mpira wa pete, mpira wa miguu, wavu, kikapo na mchezo wa bao, pamoja na kutafuta Miss na Mr TIA, wachekeshaji, waigizaji, wabunifu na wajasiriamali inahusika na siku ya kilele Mei 21,2022 zawadi zitatolewa kwa washindi.
/*** Collapse the mobile menu - WPress Doctor ****/