MFAMASIA MKUU WA SERIKALI NA MKURUGENZI WA HUDUMA ZA DAWA TANZANIA AIPONGEZA TIA KWA KUBADILISHA CHANGAMOTO KUWA FURSA KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

November 25, 2021
Mfamasia Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa huduma za dawa Tanzania Ndg. Daud Msasi leo,ameipongeza TIA kwa kuibadilisha changamoto kuwa fursa katika utunzaji wa stoo na ugawaji wa dawa kwa Hospitali za Rufaa na Kanda.
“TIA nawapongeza sana kwa kuwa Wabunifu katika kuona Changamoto gani zinaikabili Jamii na kuichukua kama fursa  ili kutatua tatizo, kumekuwa na changamoto kubwa sana katika kurekodi dawa zilizoingia na zinazotoka, hali ambayo inapelekea wananchi kutopata huduma stahiki na kwa wakati,”. Alisema Mfamasia Mkuu wa Serikali
Aidha, Ndg. Daud Msasi amesema ni imani yake kubwa kuwa watumishi hao kutoka katika Hospitali za Serikali wataenda kutoa huduma bora Kwa Wananchi kwani tayari wana mafunzo ya Kutosha na hategemei mtumishi yoyote yule aliyehudhuria mafunzo hayo kwenda kurudia makosa yale yale ya nyuma katika utunzaji na ugawaji dawa.
Ameongeza kuwa anayo orodha ya watumishi wote waliopata mafunzo na atahakikisha anapita kwa kila kituo cha kazi cha mshiriki kukagua kama wanafuata taratibu walizofundishwa katika kutoa huduma za dawa.
Mfamasia Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa huduma za dawa amesema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya Wafamasia, watalaam wa maabara na maafisa ugavi wapatao 40 yaliyofanyika Mkoani Morogoro na kuwatunuku Cheti cha kufuzu mafunzo hayo.
Naye Bi.Clementina Salutari ameishukuru Taasisi ya Uhasibu Tanzania kwa niaba ya washiriki wenzake kwa kuwapa elimu iliyozingatia tafiti na ushauri ambayo inaenda kuboresha utoaji wa huduma za Afya hususani katika utunzaji na ugawaji wa dawa, pia wametoa shukrani zao za dhati kwa Taasisi walizotoka kwa kupewa ruhusa kushiriki mafunzo hayo yenye tija kubwa kwa jamii wanayoihudumia.
Mafunzo hayo yametolewa na wakufunzi mahiri waliobobea katika Manunuzi na Ugavi kutoka TIA Kampasi ya Mbeya akiwemo Ndg.Nyandwi Mrihano, Ndg.Alfred Manda, Ndg.Francis Msangi kwa kushirikiana na mratibu Ndg. Boyd Mwanyumba.
TIA itaendelea kutoa tafiti na ushauri wenye kuleta matokeo chanya kwa Jamii.
/*** Collapse the mobile menu - WPress Doctor ****/