Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Eve Godwin Mkini, ambaye pia ni Miss TIA 2026, amepata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Africa International yatakayofanyika nchini Nigeria mwezi Oktoba mwaka huu.
Miss Mkini ametoa shukrani hizo leo katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Makao Makuu jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa msaada na mazingira aliyoyapata TIA vimemwezesha kukuza kipaji chake huku akiendelea na masomo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William A. Pallangyo, amempongeza Miss Mkini kwa hatua hiyo na kumtaka kujiandaa vizuri kwa mashindano hayo, hususani katika kujibu maswali, ubunifu, maadili, mavazi na kuzingatia tamaduni za Kiafrika.
Prof. Pallangyo pia amewahimiza wanafunzi wa TIA kutambua na kutumia vipaji vyao, akisisitiza umuhimu wa kutumia fursa zinazopatikana ndani na nje ya taasisi katika kujenga uwezo na kujiamini.
Kwa upande wake, Miss Mkini ameahidi kufanya vizuri na kuitangaza Tanzania nchini Nigeria, huku akiwahamasisha vijana wenye vipaji mbalimbali kujiamini, kuviendeleza na kuchangamkia fursa zinazowazunguka.





















