Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki mkutano wa Waratibu wa Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) unaofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mkutano huo wa siku tatu unalenga kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi pamoja na maandalizi ya hatua za mwisho kuelekea kufungwa rasmi kwa mradi huo mwezi Julai 2026.
Washiriki kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini wamekutana kujadili mafanikio, changamoto pamoja na mikakati ya kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa wakati.
Katika mkutano huo, TIA kupitia kwa Magreth Emmanuel, Mratibu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa HEET-TIA, imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mradi huo, ikiwemo maboresho ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, maendeleo ya mifumo ya kidijitali pamoja na kuimarishwa kwa mazingira ya utoaji wa mafunzo.
Aidha, washiriki wamejadili masuala ya usimamizi wa fedha, manunuzi, ujenzi, mafunzo kwa watumishi pamoja na maandalizi ya tathmini za mwisho za mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Mradi wa HEET unalenga kuimarisha ubora wa elimu ya juu nchini kwa kuboresha miundombinu, kuongeza matumizi ya teknolojia pamoja na kuimarisha uwezo wa rasilimali watu ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa.

























