Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William A. Pallangyo, amesaini mikataba ya makubaliano ya mashirikiano na kampuni tatu: JM Investment, Tukiio, na Basil Link Company Ltd, kwa ajili ya maandalizi ya TIA Marathon msimu wa pili leo tarehe 04 Septemba, 2025
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Prof. Pallangyo amesema kuwa lengo kuu la TIA marathoni ni kukuza afya, kuimarisha mshikamano, na kuhamasisha uwekezaji katika elimu bora kwa vijana wa Kitanzania.
“Lengo letu ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wasiojiweza, wakiwemo mabinti waliopata ujauzito wakiwa katika umri mdogo, watu wenye ulemavu kwa kuwapatia vifaa kama viti mwendo, pamoja na wale wenye uoni na usikivu hafifu,”alisema Prof. Pallangyo.
Aidha, alieleza kuwa marathoni hiyo ni fursa ya jamii kuungana, kuhamasika, na kuonyesha kuwa elimu na afya ni mambo yanayokwenda pamoja.