Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), imeandaa Kongamano la tatu (3) la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi linaloendelea jijini Arusha, ambalo limeanza jana tarehe 7 hadi 9 Novemba, 2024.
Kongamano hilo limehusisha watafiti, wataaluma, Wadau wote wa uchumi na Biashara toka ndani na nje ya nchi.
Wakati akifungua Kongamano hilo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu, Mhe Doto Biteko, (MB) amesema watafiti wanatakiwa kufanya tafiti zenye tija na kutoa matokeo ya tafiti zao ili ziwanufaishe wananchi katika kuhakikikisha changamoto za jamii zinatatuliwa sambamba na kukuza uchumi.
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (MB) amesema ni wakati muafaka wa tafiti zinazotolewa na wataalamu hao kuanza kuzitumia kudadavua kwa kina juu ya mwelekeo wa uchumi haswa katika ubunifu wa biashara na uchumi hususani katika tafiti atamizi.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Profesa Jehovaness Aikael amesema watafiti lazima kuendelea kufanya tafiti zaidi katika uwekezaji, usimamizi wa biashara ndani na nje ya nchi ili kuimarisha uchumi na uboreshaji mazingira ya biashara na kufikia malengo ya milenia.
Pia Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Profesa William Pallangyo amesema TIA itaendelea kufanya tafiti ambazo zinagusa jamii na taifa kwa ujumla hususani tafiti zinazogusa maendeleo ya uchumi na biashara katika uwekezaji.