Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ametembelea na kukagua ujenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Kampasi ya Mwanza, inayojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha, kwa gharama ya shilingi bilioni 7.8, kitakachokuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi zaidi ya 5,000 kwa wakati mmoja,
“Afisa Mtendaji Mkuu umefanya kazi nzuri sana, majengo ya Kampasi ya TIA Mwanza yamejengwa katika viwango ambavyo Serikali ya awamu ya sita inataka, sikutegemea kufanyika kwa kazi nzuri namna hii, hapa Mtendaji Mkuu na menejimenti mnastahili pongezi,”. Alisema Dkt. Mwigulu Naye,
Afisa Mtendaji Mkuu Profesa William Pallangyo, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali kupitia Wizara ya Fedha, imeipatia TIA shilingi za kitanzania bilioni 58.1 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika Kampasi za Mtwara bilioni 6.1, Mbeya bilioni 3.2, Mwanza bilioni 7.8, Kigoma bilioni 11 na Zanzibar bilioni 30,
“Kwa sasa, mradi wa Kampasi ya Mwanza umekamilika kwa asilimia 99 na unatarajia kuzinduliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 12 Oktoba, 2024,”. Alisema Profesa Pallangyo
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mhe. Machibya Kashinje amesema wananchi wa Misungwi wamepokea mradi wa TIA kwa furaha kubwa ya wanafunzi kupata elimu ya juu katika mazingira mazuri na ya kisasa. “Ujenzi wa TIA Kampasi ya Mwanza Mhe. Waziri umefungua fursa nyingi sana hususani za elimu na uchumi kwa wakazi wa Misungwi, na kanda ya ziwa kwa ujumla,”. Alisema Mwenyekiti Machibya
Mwananchi Joseph Majula, amesema ujio wa Kampasi ya TIA binafsi umempa fursa ya kupeleka vijana wake wawili kuanza cheti cha awali, na mmoja amechaguliwa kujiunga TIA kozi ya Ugavi na Ununuzi. Halikadhalika, Waziri Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipanda miti ikiwa ni kiashiri ya utunzaji mazingira.