TIA watakiwa kutekeleza Dira ya Taasisi

May 8, 2022

Wafanyakazi na wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania(TIA), wametakiwa kutambua na kuifuata dira ya Taasisi na kuitekeleza ili kuweza kufikia malengo ya kuwa Taasisi inayotoa elimu yenye ubora katika biashara,huduma za utafiti na ushauri barani Afrika.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo wakati akizungumza katika Baraza la Wanafunzi wa TIA lililofanyika leo, Jijini Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kwa wanafunzi kuzingatia misingi na kanuni ya Taasisi   wakisaidiwa na wahadhiri ambao ndio wasimamizi wakuu kuhakikisha dira hiyo inatekelezwa kwa vitendo.

“Wahadhiri tuendelee kusimamia taaluma  ili tuweze kutoa mazao bora zaidi kulingana na masomo tunayotoa ili wahitimu wetu wakifika makazini huko wawe na ubora uliopikwa ukapikika ,”. alisema Profesa Pallangyo

” Taasisi ina misingi sita ya maadili ambayo ni ubora,uwajibikaji,weledi, ubunifu , uadilifu na ushirikiano na tuhakikishe ubora unazingatiwa na hapa wahadhiri ndio msingi wa jukumu lenu kuhakikisha tunapeleka bidhaa bora sokoni,”. alisisitiza Profesa Pallangyo

Pia amewaasa wanafunzi kutumia vipaji walivyonavyo katika kutimiza malengo yao huku akitoa angalizo kutosoma ili utafute ajira bali uwe tayari hata kujiajiri kwa kutoa ushauri wa kitaalamu kama kada zingine zinazotoa ushauri wa kitaalamu kwenye vikundi mbalimbali.

“Mwanafunzi usiwe job seeker bali uwe na uwezo wa kujiajiri na kuwa msaada katika jamii yako mfano wewe ni mhasibu uwe unasaidia SACCOS za mtaani kwako,”. Alisema Profesa Pallangyo

Wakati huo huo amempongeza Dkt. Momole Kasambala aliyekuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TIA kwa kazi nzuri aliyoifanya pamoja na Uongozi Mzima wa TIASO (Serikali ya Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu) huku akiahidi kufanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na kuhakikisha wanafunzi wanapata mrejesho kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia ili wapate elimu kwa furaha.

/*** Collapse the mobile menu - WPress Doctor ****/