Taasisi ya Uhasibu Tanzania imedhamiria kuwa Taasisi inayotoa elimu yenye ubora katika biashara, huduma za Utafiti na ushauri barani Afrika kwa kuboresha mazingira ya usomaji na ufundishaji ili kuendana na kasi ya teknolojia.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Dkt.Momole Kasambala katika ufunguzi wa kikao cha Nne cha Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi kilichofanyika Ukumbi wa Kampsi ya TIA Singida.
Dkt.Kasambala amesema Taasisi imeendelea kutimiza majukumu yake katika kuchangia Maendeleo ya Taifa kwa kutoa huduma ya ushauri kwenye nyanja bobezi katika kuchangia ukuaji wa Uchumi wa Viwanda Nchini.
Pia TIA imeendelea kutoa mafunzo kwenye baadhi ya Taasisi za Serikali ikiwemo Halmashauri na Hospitali za Rufaa ili kuboresha huduma za Jamii na kuwezesha Taasisi hizo kuibua vyanzo vipya vya mapato na kudhibiti upotevu wa mapato hayo.
Dkt.Kasambala amesema jitihada za Wafanyakazi ambao wameendelea kufanya Kazi kwa bidii na kwa moyo wa kujituma imeleta tija kubwa kwani idadi ya Wanachuo imeongezeka kutoka 21,736 mpaka kufikia Wanachuo 24,331
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi wote wa TIA kwa kuchapa kazi na kutekeleza kauli mbiu Ya TANZANIA IMARA, KAZI IENDELEE kwa Vitendo,”. Amesema Afisa Mtendaji Mkuu
Kwa upande wa miundombinu, Dkt. Kasambala amesema TIA inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika Kampasi ya Mtwara kwa “force account” ambapo miradi hiyo inatekelezwa kwa vyanzo vya mapato ya ndani, ikiwa ni ujenzi wa Maktaba na Maabara ya Kompyuta, Madarasa, Bweni la Wanawake, Bweni la Wanaume na Nyumba ya Watumishi yenye uwezo wa kuchukua familia mbili.
Dkt. Kasambala amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeanza ujenzi wa jengo la Taaluma katika Kampasi ya Mwanza ambalo litakuwa na Maabara ya Kompyuta na Maktaba, Ofisi ya Wafanyakazi pamoja na Madarasa.
“Mradi huu umeanza mwezi desemba 2021 na unatarajiwa kukamilika desemba 2023,”. Amesema Dkt.Kasambala
Taasisi ya Uhasibu Tanzania itatumia fursa zilizopo katika jamii na kufanya tafiti na kutoa ushauri wenye tija kwa maslahi ya Taifa.