Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), yapongezwa kwa utoaji wa mafunzo yanayowaandaa wahitimu kukidhi mahitaji ya soko kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda, na ukuaji wa Teknolojia.
Rai hiyo imetolewa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Leonard Mkude, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa mahafali ya 19 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyohusisha Kampasi ya Dar es Salaam na Mtwara yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Bw. Mkude alisema wahitimu wakijengewa uwezo vizuri watakua kwenye nafasi nzuri ya kushindana katika soko la ajira dunia lakini pia wataweza kujiari.
“Nawapongeza kwa kuendelea kuwajengea uwezo wananchi wa sekta mbalimbali kupitia mafunzo na huduma za ushauri zinazotolewa na Taasisi yenu”alisema Bw. Mkude.
“Tuendelea kubuni mbinu zaidi katika utoaji huduma za utafiti na ushauri kwa kuwa zina mchango mkubwa katika kuzalisha mapato ya nchi,” aliongeza Bw. Mkude.
Alisema kuwa ufanyaji wa tafiti huisaidia Serikali kupata majawabu ya changamoto mbalimbali ambazo Taifa linakabiliana nazo katika jitihada za kuimarisha uchumi.
Aliitaka TIA, kuendelea kujitangaza ili kuweza kuwafikia wananchi wa kawaida hususan waliopo kwenye maeneo ya pembezoni, ili watambue na kunufaika na fursa za mafunzo, utafiti na ushauri mbalimbali unaotolewa na Taasisi hiyo.
Aidha alitoa wito kwa wahitimu hao kutumia elimu walioipata kama chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira.
Bw. Mkude aliwaasa wakienda makazini kuhakisha wanafanya kazi kwa bidii, uadilifu, ubunifu, umakini, weledi na kujiepusha na uzembe kwa kuzingatia Sera, Sheria, Taratibu na Kanuni mahali pakazi.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Taasisi ya Uhasibu Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu nchini zinazotoa mafunzo kwa viwango vya Kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Wizara ya Fedha na Mipango Wakili Said Musendo Chiguma, alisema kuwa wahitimu wa TIA wamekuwa na utendaji kazi uliotukuka katika Sekta za Umma na Binafsi tumekuwa tukipata mrejesho kupitia waajiri mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa hali hiyo imepelekea kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi mwaka hadi mwaka licha ya kuwepo vyuo vingi vya ushindani ambapo Taasisi inajumla ya wanafunzi 25,249 ikiwa ni ongezeko la asilimia 71 kutoka wanafunzi 14,800 la mwaka 2016.
Dkt. Kasambala amesema TIA imefanikiwa kuanzisha Kozi za Shahada ya Uzamili zipatazo 5, ikiwemo Shahada ya Sayansi katika Uhasibu na Fedha, katika Ugavi na Ununuzi, Ubunifu katika Usimamizi wa Miradi, Uongozi na Rasilimali Watu na Tehama pamoja na Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Masoko na Uhusiano wa Umma.
Aliongeza kuwa pia TIA imefanikiwa kuanzisha mashirikiano na vyuo nane vya nje vikiwemo Vyuo Vikuu vya India, Ukraine na Kenya ambapo hatua hiyo itawezesha Wahadhiri na Wanachuo kuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu ili kuleta tija kupitia mashirikiano hayo.
Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Uhasibu yamejumuisha wahitimu 7,131 kutoka Kampasi ya Dar es Salaam na Mtwara yenye jumla Wanawake 3,677 sawa na asilimia 51.6 ya wahitimu wote, na Wanaume 3,454 sawa na asilimia 48.4 ya wahitimu wote, wahitimu hao wametunukiwa Cheti cha Awali, Astashahada, Stashahada, Shahada na Stashahada ya Uzamili.