TANZANIA INSTITUTE OF ACCOUNTANCY

TARI NA TIA WASAINI MKATABA WA MASHIRIKIANO JIJINI DODOMA

October 27, 2022

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. William A. Pallangyo pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dkt. Geoffrey S. Mkamilo wamesaini Makubaliano ya Mashirikiano  baina ya Taasisi hizo mbili ya kuwajengea uwezo watafiti wa TARI, wahadhiri na wafanyakazi waendeshaji wa TIA sambamba na  Wanachuo wa TIA.

Makubaliano hayo ambayo yameshuhudiwa na baadhi ya Watumishi wa taasisi hizo wakiwemo Makamu Mkuu wa Chuo- Mipango, Fedha na Utawala wa TIA Dkt. Issayah Hassanali na Mkurugenzi wa Utafiti TARI Profesa Joseph Ndunguru yamefanyika leo tarehe 26 Oktoba 2022 katika Ofisi za Taaasisi ya TARI, Makutupora, Dodoma.

Dkt. Mkamilo amesema, kwa sasa kilimo ni biashara,  hivyo tafiti za TARI lazima zilenge katika ubunifu wa mbegu bora na teknolojia inayogunduliwa  lazima iwafike walaji mapema kwa maendeleo endelevu ya kilimo.

” Utekelezaji wa Makubaliano ya mashirikiano haya, utaanza mapema ili kuleta manufaa kwa pande zote, kwa maendeleo ya jamii  ya Watanzania”. Alisisitiza Dkt. Mkamilo

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Profesa William Pallangyo amesema, Mashirikiano haya yana manufaa kwa taasisi hizi mbili kwa kuwa kupitia maeneo ya mashirikiano Wanachuo wa TIA watapata fursa za kujifunza na wahadhiri watapata nafasi ya kutoa mafunzo kwa watafiti wa TARI.

Taasisi ya Uhasibu Tanzania ( TIA) imelenga kuendelea kufanya tafiti zenye tija kwa maendeleo ya Watanzania katika makundi mbali mbali yakiwemo wajasiriamali wadogo wadogo, Wakulima na Wafugaji.

/*** Collapse the mobile menu - WPress Doctor ****/