Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Prof. William A. Pallangyo, leo tarehe 27/04/2022 amefungua mafunzo ya siku tatu ya Usimamizi wa Mikataba na Miradi kwa Watumishi  wa TIA ambao kwa nafasi zao ni wadau muhimu katika kusimamia masuala ya Mikataba na Miradi.
Wakati akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Adem, Bagamoyo, Prof. Pallangyo amesema mafunzo haya yana umuhimu  hususani katika kipindi hiki ambacho Taasisi inaendelea na utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya ujenzi wa Miundombinu katika Kampasi za Mtwara, Mwanza, Kigoma, Mbeya, Singida na maboresho makubwa ya miundombinu yanayoendelea katika kampasi ya Dar es Salaam.
Pia Prof. Pallangyo amesema wakati Taasisi inaelekea kuongeza wigo wa utoaji huduma  nje ya Tanzania Bara katika visiwa vya Unguja, Zanzibar
“Ni lazima TIA ionekane tofauti ikiwa na majengo yaliyojengwa kitaalamu, pia tuingie Mikataba ambayo ni sahihi na utekelezaji wake ufanyike kwa wakati,”. Amesema Prof. pallangyo
Aidha, Prof. Pallangyo aliongeza kuwa mada zitakazofundishwa zina tija kubwa katika utekelezaji wa miradi
“Tunategemea tukirudi ofisini tuwe na mabadiliko makubwa ili  thamani ya pesa na gharama zilizotumika kwenye mafunzo haya iweze kuonekana na pia tuhakikishe tunagema kutoka kwa huyu mtaalamu,”. Amesisitiza Prof. Pallangyo
Mafunzo ya usimamizi wa mikataba na miradi yanayoendeshwa na mtalaamu mbobezi Mhandisi Paul F. Basondole yanasimamiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Hassanal Issaya na kuratibiwa  na Meneja Miliki wa TIA Mhandisi Masuhuko Nkuba.
“TIA -Elimu kwa Ufanisi”