Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William A. Pallangyo, leo tarehe 03 Desemba 2024, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya taaluma katika Kampasi ya Kigoma. Mradi huo, unaoendelea katika eneo la Kamala lenye hekari 56, unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 11 hadi kukamilika.
Akiwa katika ziara hiyo, Prof. Pallangyo amesema ujenzi huu unatarajiwa kuchukua zaidi ya wanafunzi 1,500 kwa wakati mmoja. Miundombinu itajumuisha ofisi 25, kumbi za mihadhara, maktaba, na maabara ya kompyuta, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Prof. Pallangyo ameagiza mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa, huku akibainisha kuwa utakamilika kabla ya kuanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026. Amesisitiza kuwa wakazi wa Kigoma na mikoa jirani wachangamkie fursa hii ya kipekee kwa ajili ya elimu yenye ufanisi inayotolewa na TIA.
Ziara hiyo iliambatana na viongozi mbalimbali, wakiwemo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Fedha, Mipango na Utawala, Dkt. Issaya Hassanal, Mkurugenzi wa Kampasi ya Kigoma, Dkt. Florence Sitima, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko, Bi Lillian Rugaitika. Maafisa wengine kutoka Kampasi za Kigoma na Dar es Salaam pia walihudhuria.
Mradi huu unaakisi juhudi za TIA katika kuboresha elimu na miundombinu ya taasisi, huku ukiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.