Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Dkt. Leonada Mwagike (ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Taaluma), Bw.Thabit Dokodoko (Mwenyekiti Kamati ya Ukaguzi) na  Bi.Emma Lyimo (Mjumbe Kamati ya Taaluma) leo tarehe 13/02/2023 wametembelea Mradi wa Ujenzi wa Kampasi ya Mwanza unaoendelea Kata ya Nyangh’omango, Wilaya ya Misungwi.
Akifafanua maendeleo ya huo msimamizi wa Mradi Msanifu Ujenzi Godfrey Seni amesema ujenzi umekamilika kwa 68% ikiwa ni asilimia 15% mbele, ambapo amebainisha kuwa gharama ya Mradi ni shilingi Bilioni 7.8 ambazo zinagharamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa pamoja wajumbe wa bodi hiyo  wameipongeza Menejimenti ya TIA na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kugharamia Mradi huo mkubwa  ambao unatarajiwa kukamilika  tarehe 24/01/2024.
Mradi huo unajumuisha jengo la Mihadhara, Maabara ya Kompyuta na Maktaba, pamoja na jengo la Utawala ambalo litakuwa na Ofisi za Wahadhiri, Wafanyakazi Waendeshaji na Ukumbi wa Mikutano, hayo yalielezwa na Mhandisi Nkuba wakati akisoma taarifa ya maendeleo ya mradi.
Kukamilika kwa Mradi huo kutawezesha Taasisi kuhama kwenye majengo ya kupanga ili kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, kuongeza idadi ya udahili kufuatia ongezeko kubwa la wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na sita kutokana na sera ya Serikali ya elimu bure.
Aidha, uwepo wa Mradi huo umefungua ajira za aina mbili ikiwemo ajira ya kudumu kwa wafanyakazi wajenzi na ajira za muda mfupi ambapo kwa siku jumla ya vibarua 140 wamekuwa wakiajiriwa kwa wastani.
Ziara hiyo, iliongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Prof. William A. Pallangyo, aliyefuatana na Makamu Mkuu wa Chuo- Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Dkt. Momole Kasambala, Meneja wa Kampasi ya Mwanza Dkt. Honest Kimario. Meneja Miliki Mhandisi Masuhuko Nkuba na Mkuu wa Masoko na Uhusiano Bi. LIlian Mpanju Rugaitika.
Kazi Iendelee