TANZANIA INSTITUTE OF ACCOUNTANCY

NAIBU WAZIRI AWAASA VIJANA MATUMIZI SAHIHI YA TEKNOLOJIA

November 16, 2022

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango  Mhe.Hamad H. Chande (MB) amewaasa wahitimu kutumia teknolojia ya mawasiliano katika kujiletea tija kwenye maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla, kumekuwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo yanaharibu maisha ya vijana wengi, baadhi ya vijana wamekosa ajira kwa makosa ya kimaadili waliyoyafanya kwenye mitandao hiyo.

Mhe. Chande amesema hayo wakati akiwatunuku  wahitimu 2,352 wa Kampasi ya Mbeya ambao ni sawa na asilimia 17.3 ya wahitimu wote, wakiwemo wanawake 1,266 sawa na asilimia 53.8 na wanaume 1,086 sawa na asilimia 46.2, nawapongeza kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapa fursa wanawake pasipo ubaguzi.

”  Napenda kuwapongeza sana kwa kuhitimu rasmi mafunzo yenu leo, safari yenu ya mafunzo ilikuwa ndefu, mmekabiliana na changamoto za hapa na pale lakini wengi wenu mmeweza kutimiza ndoto zenu, mmedhihirisha umahiri wenu, na kutupa wasaa wa kushuhudia matunda ya juhudi zenu, hongereni sana,”. Amesema Mhe. Chande

Aidha, Naibu Waziri amesema amefurahishwa na TIA kuona inafanyia kazi maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu kwa kutoa elimu ujuzi ili kuwawezesha wanachuo kujiajiri na kuendelea kuzingatia kwa umakini suala la umahiri katika mitaala  ili kupata wataalam wenye uwezo wa kuleta mabadiliko kiuchumi,

” Katibu Tawala wilaya ya Mbeya uwachukue vijana wenye ubunifu wa uzalishaji Chaki na Mafuta ya kupikia uwaunganishe na Halmashauri wapate mikopo ili wakamilishe ndoto .” Amesema Mhe. Chande

Pia Mhe. Chande amesema hatua waliyofikia wahitimu hao ni chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma, Serikali inajitahidi kufungua wigo wa ajira ingawa Soko letu la ajira rasmi ni dogo sana na halikidhi mahitaji ya wahitimu wote nchini, ili kukabiliana na changamoto hiyo ni vyema mkaelekeza mawazo yenu kwenye kujiajiri badala ya kuajiriwa.

Mahafali hayo ni ya 20 na ya 10 kufanyika Kampasi ya Mbeya yamehudhuriwa na wadau mbalimbali akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Chifu wa Wasafwa, Naibu Meya wa Jiji la Mbeya, Taasisi za Kiserikali na sizizo za kiserikali, Wazazi, Walezi na Wahitimu.

 

/*** Collapse the mobile menu - WPress Doctor ****/