TANZANIA INSTITUTE OF ACCOUNTANCY

MKURUGENZI IDARA YA MIPANGO, WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO ATEMBELEA KAMPASI TARAJIWA YA TIA  ZANZIBAR 

March 11, 2023

Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Moses Dulle mapema wiki hii amefanya ziara katika Kampasi tarajiwa ya TIA, iliyopo eneo la Makunduchi Zanzibar kwa lengo la kukagua eneo la ujenzi wa Kampasi hiyo na kuweka mipango inayoendana na mazingira halisia.

Bw. Dule aliambatana na Maafisa Mipango Ramadhani Kipambe na Morgan Simkanga ambapo ziara hiyo ilianzia kwenye Afisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe. Rajab Mkasaba ambaye alipongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kuona umuhimu wa kuanzisha tawi la TIA wilayani humo.

Mkasaba alisema wananchi watanufaika na huduma za mafunzo, utafiti na ushauri wa kitaalam zitolewazo na TIA kwa ufanisi mkubwa huku akisisitiza umuhimu wa mashirikiano na kuanza ujenzi mapema.

TIA inategemea kuanza kutoa huduma za mafunzo rasmi mnamo Mwezi Septemba 2023.

Kwa sasa maandalizi ya awali ya ujenzi yameanza.

Kwa upande wa TIA walioshiriki ziara hiyo ni pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu (TIA) Prof. William A. Pallangyo akifuatana na Makamu Mkuu wa Chuo- Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Issaya Hassanal, Meneja Miliki Mhandisi Masuhuko Nkuba, Mkuu wa Masoko na Uhusiano Lillian Mpanju Rugaitika na Afisa Utumishi Mkuu Thomas Mabeba.

Kampasi ya Zanzibar itakuwa kampasi ya Saba, huku kampasi nyingine zikiwa katika Mikoa ya Dar es Salaam (makao makuu), Mbeya, Singida, Mtwara, Mwanza na Kigoma, zikiwa na jumla ya wanachuo wapatao 26,463 katika kozi za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Raslimali Watu, Masoko na Uhusiano  wa Umma, Uhasibu wa Umma na Fedha, Usimamizi wa Fedha na Usimamizi wa Miradi katika ngazi ya Cheti cha Awali, Astashahada, Stashahada, Stashahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamili.

Kazi Iendelee

/*** Collapse the mobile menu - WPress Doctor ****/